.Kamimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi akitoa taarifa ya masuala mbalimbali yahusuyo Bodi yake mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Profesa Jumanne Maghembe wakati wa mkutano na Menejimenti ya TTB leo. Kulia kwa Bi Devota ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Agelina Madata
Wajumbe wa Menejimenti ya TTB wakimsikiliza kwa
makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani (wa pili kulia katika meza
kuu) leo jijini Dar es
salaam.
---
Waziri wa Maliasili
na Utalii Profesa Jumanne Maghembe (MB) ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania- TTB
kuendelea kutumia vyombo vya habari vya Kimataifa kama vile CNN, BBC n.k
kuitangaza Tanzania kama eneo la Utalii duniani sambasamba na kuweka makala na
matangazo ya utalii wetu katika majarida ya Kimataifa yanayoandika habari za
Utalii na usafiri (Travel Magazine) ambayo ndiyo husomwa na watalii wengi
duniani.
“Kama kweli
tunataka kupata watalii wengi zaidi pamoja na mambo mengine ni lazima tutumie
vyombo vikubwa vya Kimataifa vinavyofikia watu wengi zaidi duniani” alisema na
kuongeza kuwa pamoja na njia nyingine zinazotumiwa katika kuitangaza Tanzania
kimataifa, mbinu hii ya kutumia vyombo vya habari yaweza kuwa na ufanisi mkubwa
zaidi .
Waziri Maghembe
ameyasema hayo leo alipotembelea Bodi ya Utalii Tanzania na kukutana na
Menejimenti ya TTB kwa lengo la kujitambulisha na kubadilishana
mawazo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi katika utangazaji utalii ndani na
nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu
madeni makubwa yanayoikabili TTB, Mh. Profesa Jumanne Maghembe
ameahidi kuwa Wizara yake itachukua madeni yanayoikabili TTB na hasa
yaliliyotokana na maelekezo ya Wizara ya kama yale yaliyotokana na kuitaka Bodi
iingie mikataba ya kuweka matangazo katika ligi kuu ya Uingereza na klabu za
mpira wa mguu na Sunderland Football Association pia ya nchini Uingereza.
Amesema Wizara ni
lazima ilipe madeni hayo ili kulinda taswira ya Bodi ya Utalii kwa wadau na
kuiondolea Bodi mzigo wa kuhangaikia madeni hayo badala yake ijikite zaidi
katika kutangaza utalii.Kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa utalii nchini Profesa
Maghembe amebainisha kuwa pamoja na uwepo wa mashirika mbalimbali ya ndege
yanayokuja hapa nchini lakini kuna haja kubwa Tanzania kuwa na shirika lake
imara la ndege ambalo litasaidia sana kukuza utalii nchini kama ilivyo kwa nchi
nyingine kama Kenya na Afrka ya Kusini.
Aidha amesema kuna
haja pia ya kuboresha na kuendeleza zaidi vivutio vyetu vya utalii
na mazao mengine ya utalii kama vile Utalii wa fukwe na Utalii wa
utamaduni sambasamba na kukamilisha zoezi la uwekaji madaraja hoteli zetu na
kutoa elimu kwa wenye hoteli kuboresha zaidi hoteli zao na hudiuma watoazo.
Katika mkutano huo
uliohudhuriwa pia na viongozi wengine kutoka Wizarani akiwemo Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani, Naibu katibu Mkuu Bi Angelina Madata na
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Bw. Zahoro, Waziri Maghembe amesema anataka kuona
idadi ya watalii ikiongezeka kutoka 1,100,000 ya sasa na kufikia Milioni
3,000,000 mwaka 2018.
Mapema kabla ya
kumkaribisha waziri kuzungumza na Menejimenti, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Bodi ya Utalii Bi Devota Mdachi alimwelezea Mh. Waziri mafanikio kadhaa ambayo
Bodi imeyapata ikiwa ni pamoja na kuanzisha onesho la Utalii la Kimataifa la
Swahili Swahili International Tourism Expo (S!TE) linalofanyika kila mwaka
jijini Dar es salaam, kuanzishwa kwa tovuti maalumu (Portal) ya kuitangaza
Tanzania na kulipia huduma nyingine za utalii moja kwa moja , uwekaji wa
matangazo sehemu mbalimbali duniani.
Bi Devota
alimfahamisha pia Mh. Waziri kuwa TTB imechaguliwa kuwa miongoni mwa Bodi za
Utalii tatu bora barani Afrika ambazo zinashindanishwa kumpata mshindi wa
kwanza na wa pili. “Mh. Waziri, pamoja na matatizo mengi yanayoikabili TTB
lakini tunafurahi kukujulisha kuwa TTB ni miongoni mwa bodi za utalii tatu
zilizoingia katika hatua ya mwisho ya kutafuta mshindi wa Bodi ya Utalii borani
Afrika tukishindana na Bodi za utalii za Afrika ya Kusini na Namibia katika
shindano linaoendeshwa na taasisi ya Travvy ya Marekani” alidokeza Bi Mdachi.
Kaimu
Mkurugenzi huyo alidokeza pia kuhusu changamoto kadhaa zinazoikabili
Bodi kubwa zaidi ikiwa ni madeni makubwa ya nje na ndani, na bajeti ndogo ya
utangazaji.