Top Ad 728x90

Wednesday, January 6, 2016

TUMIENI VYOMBO VYA KIMATAIFA KUITANGAZA TANZANIA - WAZIRI MAGHEMBE

Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Profesa Jumanne Maghembe akizungumza na Menejimenti ya Bodi ya Utalii leo jijini Dar es salaam.
.Kamimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi akitoa taarifa ya masuala mbalimbali yahusuyo Bodi yake mbele ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Profesa Jumanne Maghembe wakati wa mkutano na Menejimenti ya TTB leo. Kulia kwa Bi Devota ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bibi Agelina Madata
Wajumbe wa Menejimenti ya TTB wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani  (wa pili kulia katika meza kuu) leo  jijini Dar es salaam.
---
Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe (MB) ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania- TTB kuendelea kutumia vyombo vya habari vya Kimataifa kama vile CNN, BBC n.k kuitangaza Tanzania kama eneo la Utalii duniani sambasamba na kuweka makala na matangazo ya utalii wetu katika majarida ya Kimataifa yanayoandika habari za Utalii na usafiri (Travel Magazine) ambayo ndiyo husomwa na watalii wengi duniani.


 “Kama kweli tunataka kupata watalii wengi zaidi pamoja na mambo mengine ni lazima tutumie vyombo vikubwa vya Kimataifa vinavyofikia watu wengi zaidi duniani” alisema na kuongeza kuwa pamoja na njia nyingine zinazotumiwa katika kuitangaza Tanzania kimataifa, mbinu hii ya kutumia vyombo vya habari yaweza kuwa na ufanisi mkubwa zaidi .




Waziri Maghembe ameyasema hayo leo alipotembelea Bodi ya Utalii Tanzania na kukutana na Menejimenti  ya TTB kwa lengo la kujitambulisha na kubadilishana mawazo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Bodi katika utangazaji utalii ndani na nje ya nchi.


Akizungumzia kuhusu madeni makubwa yanayoikabili TTB,  Mh. Profesa Jumanne Maghembe ameahidi kuwa Wizara yake itachukua madeni yanayoikabili TTB na hasa yaliliyotokana na maelekezo ya Wizara ya kama yale yaliyotokana na kuitaka Bodi iingie mikataba ya kuweka matangazo katika ligi kuu ya Uingereza na klabu za mpira wa mguu na Sunderland Football Association pia ya nchini Uingereza. 


Amesema Wizara ni lazima ilipe madeni hayo ili kulinda taswira ya Bodi ya Utalii kwa wadau na kuiondolea Bodi mzigo wa kuhangaikia madeni hayo badala yake ijikite zaidi katika kutangaza utalii.Kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa utalii nchini Profesa Maghembe amebainisha kuwa pamoja na uwepo wa mashirika mbalimbali ya ndege yanayokuja hapa nchini lakini kuna haja kubwa Tanzania kuwa na shirika lake imara la ndege ambalo litasaidia sana kukuza utalii nchini kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Kenya na Afrka ya Kusini. 


Aidha amesema kuna haja pia ya kuboresha na kuendeleza zaidi  vivutio vyetu vya utalii na mazao mengine ya utalii kama vile Utalii wa fukwe na  Utalii wa utamaduni sambasamba na kukamilisha zoezi la uwekaji madaraja hoteli zetu na kutoa elimu kwa wenye hoteli kuboresha zaidi hoteli zao na hudiuma watoazo.


Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na viongozi wengine kutoka Wizarani akiwemo Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Bw. Ramo Makani, Naibu katibu Mkuu Bi Angelina Madata na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Bw. Zahoro, Waziri Maghembe amesema anataka kuona idadi ya watalii ikiongezeka kutoka 1,100,000 ya sasa na kufikia Milioni 3,000,000  mwaka 2018.


Mapema kabla ya kumkaribisha waziri kuzungumza na Menejimenti, Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Bi Devota Mdachi alimwelezea Mh. Waziri mafanikio kadhaa ambayo Bodi imeyapata ikiwa ni pamoja na kuanzisha onesho la Utalii la Kimataifa la Swahili Swahili International Tourism Expo (S!TE) linalofanyika kila mwaka jijini Dar es salaam, kuanzishwa kwa tovuti maalumu (Portal) ya kuitangaza Tanzania na kulipia huduma nyingine za utalii moja kwa moja , uwekaji wa matangazo sehemu mbalimbali duniani.  


Bi Devota alimfahamisha pia Mh. Waziri kuwa TTB imechaguliwa kuwa miongoni mwa Bodi za Utalii tatu bora barani Afrika ambazo zinashindanishwa kumpata mshindi wa kwanza na wa pili. “Mh. Waziri, pamoja na matatizo mengi yanayoikabili TTB lakini tunafurahi kukujulisha kuwa TTB ni miongoni mwa bodi za utalii tatu zilizoingia katika hatua ya mwisho ya kutafuta mshindi wa Bodi ya Utalii borani Afrika tukishindana na Bodi za utalii za Afrika ya Kusini na Namibia katika shindano linaoendeshwa na taasisi ya Travvy ya Marekani” alidokeza Bi Mdachi.


Kaimu Mkurugenzi  huyo alidokeza pia kuhusu changamoto kadhaa zinazoikabili Bodi kubwa zaidi ikiwa ni madeni makubwa ya nje na ndani, na bajeti ndogo ya utangazaji.


0 comments:

Top Ad 728x90